10
Ndugu, nataka mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba wote walivuka salama ile bahari. Wote walibatizwa katika umoja na Mose kwa lile wingu na ile bahari. Wote walikula chakula kilekile cha kiroho, wakanywa pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe. Hata hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani. Sasa, mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao walivyotamani. Msiwe waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: “Watu waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza.” Wala tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu ishirini na tatu elfu. Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka. 10 Wala msinung'unike kama baadhi yao walivyonung'unika, wakaangamizwa na Mwangamizi! 11 Basi, mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili kutuonya sisi, ambao mwisho wa nyakati unatukabili. 12 Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke. 13 Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama. 14 Kwa hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu. 15 Naongea nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo. 16 Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo? 17 Kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote twashiriki mkate huohuo. 18 Chukueni, kwa mfano, Wayahudi wenyewe: kwao, wenye kula vilivyotambikiwa madhabahuni waliungana na hiyo madhabahu. 19 Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu kweli zaidi ya sanamu? 20 Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe ninyi muwe na ushirika na pepo. 21 Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo; hamwezi kushiriki katika meza ya Bwana na katika meza ya pepo. 22 Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani tuna nguvu zaidi kuliko yeye? 23 Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu vyote ni halali lakini si vyote vinajenga. 24 Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya mwenzake. 25 Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu; 26 maana Maandiko yasema: “Dunia na vyote vilivyomo ni mali ya Bwana.” 27 Kama mtu ambaye si muumini akiwaalikeni nanyi mkakubali kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu. 28 Lakini mtu akiwaambieni: “Chakula hiki kimetambikiwa sanamu,” basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya dhamiri, msile. 29 Nasema, “kwa ajili ya dhamiri,” si dhamiri yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni. Mtaniuliza: “Kwa nini uhuru wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine? 30 Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru Mungu?” 31 Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu. 32 Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa la Mungu. 33 Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia, bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa.