13
Masharti Kuhusu Magonjwa Ya Ngozi Yaambukizayo
1 Bwana akawaambia Mose na Aroni, 2 “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au alama nyeupe juu ya ngozi yake ambayo yaweza kuwa ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza,* Ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma, ni neno lililotumika kwa Kiebrania kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi. ni lazima aletwe kwa Aroni kuhani ama kwa wanawe, kuhani mmojawapo. 3 Kuhani atachunguza hicho kidonda kilichopo juu ya ngozi yake, na kama nywele za mahali palipo na kidonda zimebadilika kuwa nyeupe, na ikiwa kidonda kimeingia ndani ya ngozi, basi ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma. Kuhani atakapomchunguza, atamtangaza mtu huyo kuwa ni najisi kwa kawaida ya ibada. 4 Kama alama juu ya ngozi yake ni nyeupe, lakini haionekani kuwa imeingia ndani zaidi ya ngozi, na nywele kwenye alama hiyo hazijageuka kuwa nyeupe, kuhani atamtenga mtu huyo mahali pa pekee kwa siku saba. 5 Siku ya saba, kuhani atamchunguza, na kama hakuona badiliko kwenye kile kidonda na hakijaenea juu ya ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba. 6 Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama kidonda kimepungua na hakijaenea juu ya ngozi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa ni safi, ni upele tu. Ni lazima mtu huyo afue mavazi yake, naye atakuwa safi. 7 Lakini ikiwa ule upele utaenea juu ya ngozi yake baada ya yeye kujionyesha kwa kuhani na kutangazwa kuwa safi, ni lazima aende tena kwa kuhani. 8 Kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, atamtangaza kuwa najisi, kwani ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma.
9 “Wakati mtu yeyote ana ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani. 10 Kuhani atamchunguza na kama kuna uvimbe mweupe juu ya ngozi ambao umefanya nywele kuwa nyeupe, na kama kuna nyama mbichi ndani ya uvimbe, 11 ni ugonjwa sugu wa ngozi, na kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga tena kwa sababu ni najisi tayari.
12 “Ikiwa ugonjwa utakuwa umeenea kwenye ngozi yake yote kwa kadiri kuhani atakavyoweza kuona, kwamba umeenea kwenye ngozi yote ya huyo mgonjwa kutoka kichwani mpaka wayo, 13 kuhani atamchunguza, na kama ugonjwa umeenea mwili mzima, atamtangaza huyo mtu kuwa safi. Kwa kuwa mwili wote umekuwa mweupe, yeye ni safi. 14 Lakini itokeapo nyama mbichi kwenye ngozi yake, atakuwa najisi. 15 Kuhani atakapoiona hiyo nyama mbichi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hiyo nyama mbichi ni najisi, ana ugonjwa wa kuambukiza. 16 Hiyo nyama mbichi ikigeuka na kuwa nyeupe, ni lazima amwendee kuhani. 17 Kuhani atamchunguza, na kama vidonda vimekuwa vyeupe, kuhani atamtangaza mgonjwa huyo kuwa safi; kisha atakuwa safi.
18 “Wakati mtu ana jipu juu ya ngozi yake nalo likapona, 19 napo mahali palipokuwa na jipu pakatokea uvimbe mweupe, au alama yenye wekundu na weupe, ni lazima akajionyeshe kwa kuhani. 20 Kuhani atapachunguza, na kama uvimbe umezama ndani ya ngozi, na nywele zimegeuka kuwa nyeupe, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza uliojitokeza pale jipu lilipokuwa. 21 Lakini ikiwa wakati kuhani anapopachunguza pakawa hapana nywele nyeupe ndani yake, wala hakuna shimo bali pamepungua, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba. 22 Kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. 23 Lakini ikiwa ile alama haijabadilika wala kuenea, ni kovu tu kutokana na jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi.
24 “Wakati mtu ameungua kwenye ngozi yake, pakatokea alama yenye wekundu na weupe, au alama nyeupe ikaonekana penye nyama mbichi pale palipoungua, 25 kuhani ataichunguza ile alama, na kama nywele zilizoko juu yake zimegeuka kuwa nyeupe, napo pametokea shimo, basi huo ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza ambao umetokea juu ya jeraha la moto. Kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. 26 Lakini kama kuhani akichunguza na kuona kwamba hakuna nywele nyeupe kwenye alama ile, wala hakuna shimo napo pameanza kupungua, basi kuhani atamtenga kwa siku saba. 27 Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. 28 Lakini, kama alama ile haikubadilika na wala haijaenea kwenye ngozi, napo pamepungua, ni uvimbe kutokana na jeraha la moto, na kuhani atamtangaza kuwa safi; ni kovu tu kutokana na kuungua.
29 “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana kidonda juu ya kichwa au juu ya kidevu, 30 kuhani atakichunguza kile kidonda, na kama ataona kuwa kimeingia ndani, na nywele zilizoko juu yake ni njano na nyembamba, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi, kwani ni upele; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza wa kichwa au kidevu. 31 Lakini kama kuhani akichunguza aina hii ya kidonda, kionekane kuwa hakina shimo na hakuna nywele nyeusi juu yake, basi atamtenga mtu huyo kwa siku saba. 32 Siku ya saba kuhani atachunguza kidonda kile, na kama upele haujaenea, na hakuna nywele za manjano juu yake, wala hakuna shimo lolote, 33 mtu huyo ni lazima anyolewe, isipokuwa mahali palipo na ugonjwa, naye kuhani atamtenga kwa siku nyingine saba. 34 Siku ya saba kuhani atachunguza tena ule upele; ikiwa haujaenea kwenye ngozi na hakuna shimo mahali pale, kuhani atamtangaza kuwa safi. Lazima afue nguo zake, naye atakuwa safi. 35 Lakini ikiwa upele utaenea juu ya ngozi baada ya kutangazwa kuwa safi, 36 kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, kuhani hana haja ya kutazama kama kuna nywele za manjano, mtu huyo ni najisi. 37 Hata hivyo, katika uchunguzi wake akiona hapajabadilika, na nywele nyeusi zimeota juu yake, upele umepona. Yeye si najisi, kuhani atamtangaza kuwa safi.
38 “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana alama nyeupe juu ya ngozi yake, 39 kuhani atamchunguza, na kama alama hizo zina weupe uliofifia, ni vipele visivyo na madhara vilivyojitokeza kwenye ngozi; mtu huyo ni safi.
40 “Wakati mwanaume hana nywele naye ana upaa, yeye ni safi. 41 Ikiwa hana nywele kwenye ngozi ya kichwa chake, na ana upaa tangu kwenye paji, ni safi. 42 Lakini kama ana kidonda chenye wekundu na weupe kwenye kichwa chake chenye upaa, au kwenye paji la uso, ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza unaojitokeza kichwani au kwenye paji lake la uso. 43 Kuhani atamchunguza, na kama kidonda kilichovimba juu ya kichwa chake au kwenye paji la uso ni chekundu au cheupe kama ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, 44 mtu huyo ni mgonjwa, na ni najisi. Kuhani atamtangaza kuwa najisi kwa sababu ya kidonda kwenye kichwa chake.
45 “Mtu mwenye ugonjwa kama huo wa kuambukiza ni lazima avae nguo zilizoraruka, awachilie nywele zake bila kuzichana, afunike sehemu ya chini ya uso wake, na apige kelele, ‘Najisi! Najisi!’ 46 Kwa muda wote atakaokuwa na ugonjwa huo wa kuambukiza atabaki kuwa najisi. Ni lazima aishi peke yake; ni lazima aishi nje ya kambi.
Masharti Kuhusu Upele
47 “Kama vazi lolote lina maambukizo ya upele: likiwa ni vazi la sufu au kitani, 48 lolote lililofumwa au kusokotwa likiwa la kitani au la sufu, ngozi yoyote au chochote kilichotengenezwa kwa ngozi, 49 tena kama maambukizo kwenye vazi, au ngozi, au lililofumwa au kusokotwa, au kifaa chochote cha ngozi, ni rangi ya kijani au nyekundu, huo ni upele unaoenea na ni lazima kuhani aonyeshwe. 50 Kuhani atachunguza upele huo na kukitenga kifaa hicho kwa siku saba. 51 Siku ya saba atakichunguza, na kama upele umeenea kwenye nguo, au kifaa kilichofumwa au kusokotwa, au ngozi, kwa vyovyote vile itumikavyo, ni upele uangamizao, kifaa hicho ni najisi. 52 Ni lazima aichome hiyo nguo, ikiwa ni ya sufu ama kitani iliyofumwa ama kusokotwa, ama chombo chochote cha ngozi chenye maambukizo, kwa kuwa ni upele unaoangamiza; chombo chote ni lazima kichomwe moto.
53 “Lakini wakati kuhani atakapokichunguza na kuona kuwa ule upele haujaenea kwenye nguo iliyofumwa au kusokotwa, au vifaa vya ngozi, 54 ataagiza kwamba kifaa chenye maambukizo kisafishwe. Kisha atakitenga kwa siku saba. 55 Baada ya kifaa chenye maambukizo kusafishwa, kuhani atakichunguza, na kama upele haujaonyesha badiliko lolote, hata kama haujaenea, ni najisi. Kichome kwa moto, iwe upele umeenea upande mmoja au mwingine. 56 Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kuoshwa, basi atararua sehemu iliyo ambukizwa ya nguo au ngozi au kifaa kilichofumwa au kusokotwa. 57 Lakini kama ikijitokeza tena kwenye nguo au kitu kilichofumwa au kusokotwa, ama kifaa cha ngozi, kwamba ule upele unaenea, chochote chenye upele ni lazima kichomwe kwa moto. 58 Nguo, au kitu kilichofumwa au kusokotwa, au kifaa chochote cha ngozi ambacho kimesafishwa na kuondolewa upele, ni lazima kioshwe tena, nacho kitakuwa safi.”
59 Haya ni masharti kuhusu maambukizo ya upele kwenye mavazi ya sufu au kitani, yaliyofumwa ama kusokotwa, ama kifaa chochote cha ngozi, kwa ajili ya kuvitangaza kuwa safi au najisi.
*13:2 Ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma, ni neno lililotumika kwa Kiebrania kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi.