44
Maafa Kwa Sababu Ya Ibada Za Sanamu
Neno hili lilimjia Yeremia kuhusu Wayahudi wote waishio Misri, huko Migdoli, Tahpanhesi na Memfisi,* Memfisi kwa Kiebrania ni Nofu. katika nchi ya Pathrosi Pathrosi ina maana Misri ya Juu. kusema: “Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Mliona maangamizi makubwa niliyoyaleta juu ya Yerusalemu na juu ya miji yote ya Yuda. Leo imeachwa ukiwa na magofu kwa sababu ya uovu waliokuwa wameufanya. Walinikasirisha kwa kufukiza uvumba na kwa kuabudu miungu mingine ambayo kamwe wao, wala ninyi, wala baba zenu hawakuifahamu. Tena na tena, niliwatuma watumishi wangu manabii ambao walisema, ‘Msifanye jambo hili la kuchukiza ambalo nalichukia!’ Lakini hawakusikiliza wala hawakujali, hawakugeuka ili kuuacha uovu wao, wala hawakuacha kufukiza uvumba kwa miungu mingine. Kwa hiyo hasira yangu kali ilimwagika, ikawaka dhidi ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, na kuifanya ukiwa na magofu kama ilivyo leo.
“Basi hili ndilo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Kwa nini kujiletea maafa makubwa kama haya juu yenu kwa kujikatilia mbali kutoka Yuda wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, hata kujiacha bila mabaki? Kwa nini kuichochea hasira yangu kwa kile ambacho mikono yenu imekitengeneza, mkaifukizia uvumba miungu mingine huko Misri, mahali mlipokuja kuishi? Mtajiangamiza wenyewe na kujifanya kitu cha kulaania na shutumu miongoni mwa mataifa yote duniani. Je, mmesahau uovu uliotendwa na baba zenu, na wafalme na malkia wa Yuda, na uovu uliofanywa na ninyi na wake zenu katika nchi ya Yuda na barabara za Yerusalemu? 10 Mpaka leo hawajajinyenyekeza au kuonyesha heshima, wala hawajafuata sheria yangu na amri nilizoweka mbele yenu na baba zenu.
11 “Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: Mimi nimekusudia kuleta maafa juu yenu, na kuiangamiza Yuda yote. 12 Nitawaondoa mabaki ya Yuda waliokusudia kwenda Misri kukaa humo. Wote wataangamia huko Misri, wataanguka kwa upanga au kufa kwa njaa. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana, watakufa kwa upanga au njaa. Watakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha laumu na shutumu. 13 Nitawaadhibu wale waishio Misri kwa upanga, njaa na tauni kama nilivyoiadhibu Yerusalemu. 14 Hakuna hata mmoja wa mabaki ya Yuda ambaye amekwenda kuishi Misri atakayeepuka au kunusurika ili kurudi katika nchi ya Yuda, ambayo wanaitamani sana kurudi na kuishi ndani yake, hakuna hata mmoja atakayerudi isipokuwa wakimbizi wachache.”
15 Kisha wanaume wote ambao walijua kwamba wake zao walikuwa wakifukiza uvumba kwa miungu mingine, pamoja na wanawake wote waliokuwako, yaani, kusanyiko kubwa na watu wote walioishi nchi ya Misri na Pathrosi, wakamwambia Yeremia, 16 “Hatutausikiliza ujumbe uliotuambia katika jina la Bwana! 17 Hakika tutafanya kila kitu tulichosema tutakifanya: Tutafukiza uvumba kwa Malkia wa Mbinguni na tutammiminia sadaka zetu za kinywaji kama vile sisi na baba zetu, wafalme wetu na maafisa wetu tulivyofanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Wakati ule tulikuwa na chakula tele, tulikuwa matajiri wala hatukupata dhara lolote. 18 Lakini tangu tulipoacha kumfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka za kinywaji, hatupati chochote, na tumekuwa tukiangamizwa kwa upanga na njaa.”
19 Wanawake wakaongeza kusema, “Wakati tulipomfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka zetu za kinywaji, je, waume zetu hawakujua kwamba tulikuwa tukitengeneza maandazi kwa mfano wake, na kummiminia yeye sadaka za kinywaji?”
20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake waliokuwa wakimjibu, 21 “Je, Bwana hakukumbuka na kufikiri juu ya uvumba uliofukizwa katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu na ninyi pamoja na baba zenu, wafalme wenu, maafisa wenu na watu wa nchi? 22  Bwana alipokuwa hawezi kuendelea kuvumilia matendo yenu maovu na mambo ya machukizo mliyoyafanya, nchi yenu ilikuwa kitu cha kulaania na kuachwa ukiwa pasipo wakazi, kama ilivyo leo. 23 Kwa sababu mmefukiza uvumba na kufanya dhambi dhidi ya Bwana, nanyi hamkumtii wala kufuata sheria yake au amri zake au maagizo yake, maafa haya yamekuja juu yenu, kama mnavyoona sasa.”
24 Kisha Yeremia akawaambia watu wote, pamoja na wanawake, “Sikieni neno la Bwana, enyi watu wote wa Yuda mlioko Misri. 25 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Ninyi na wake zenu mmeonyesha kwa matendo yenu kile mlichoahidi mliposema, ‘Hakika tutatimiza nadhiri tulizoziweka za kumfukizia uvumba na kummiminia sadaka za kinywaji Malkia wa Mbinguni.’
“Endeleeni basi, fanyeni yale mliyoahidi! Timizeni nadhiri zenu! 26 Lakini sikieni neno la Bwana, enyi Wayahudi wote mnaoishi Misri: ‘Ninaapa kwa Jina langu lililo kuu,’ asema Bwana, ‘kwamba hakuna hata mmoja atokaye Yuda anayeishi popote Misri ambaye kamwe ataomba tena kwa Jina langu au kuapa, akisema, “Hakika kama Bwana Mwenyezi aishivyo.” 27 Kwa maana ninawaangalia kwa ajili ya madhara, wala sio kwa mema. Wayahudi walioko Misri wataangamia kwa upanga na njaa, hadi wote watakapoangamizwa. 28 Wale watakaonusurika upanga na kurudi katika nchi ya Yuda kutoka Misri watakuwa wachache sana. Ndipo mabaki wote wa Yuda waliokuja kuishi Misri watakapojua ni neno la nani litakalosimama, kwamba ni langu au lao.
29 “ ‘Hii itakuwa ndiyo ishara kwenu kwamba nitawaadhibu mahali hapa, asema Bwana, ili mpate kujua kuwa onyo langu la madhara dhidi yenu hakika litatimizwa.’ 30 Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Nitamtia Farao Hofra mfalme wa Misri mikononi mwa adui zake wanaoutafuta uhai wake, kama vile nilivyomtia Sedekia mfalme wa Yuda mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, adui aliyekuwa akiutafuta uhai wake.’ ”

*44:1 Memfisi kwa Kiebrania ni Nofu.

44:1 Pathrosi ina maana Misri ya Juu.