34
Kifo Cha Mose
1 Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani, 2 Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi,* Yaani Bahari ya Mediterania. 3 Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari. 4 Kisha Bwana akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”
5 Naye Mose mtumishi wa Bwana akafa huko Moabu, kama Bwana alivyokuwa amesema. 6 Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo. 7 Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika. 8 Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.
9 Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.
10 Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso, 11 aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Bwana alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote. 12 Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.