Zaburi 34
Sifa Na Wema Wa Mungu
Zaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka.
1 Nitamtukuza Bwana nyakati zote,
sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote.
2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,
walioonewa watasikia na wafurahi.
3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,
akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,
nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,
akamwokoa katika taabu zake zote.
7 Malaika wa Bwana hufanya kituo
akiwazunguka wale wamchao,
naye huwaokoa.
8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,
heri mtu yule anayemkimbilia.
9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,
kwa maana wale wamchao
hawapungukiwi na chochote.
10 Wana simba wenye nguvu
hutindikiwa na kuona njaa,
bali wale wamtafutao Bwana
hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,
nitawafundisha kumcha Bwana.
12 Yeyote kati yenu anayependa uzima
na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,
na midomo yake kutokana na kusema uongo.
14 Aache uovu, atende mema,
aitafute amani na kuifuatilia.
15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
16 Uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu,
ili kufuta kumbukumbu lao duniani.
17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,
huwaokoa katika taabu zao zote.
18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,
na huwaokoa waliopondeka roho.
19 Mwenye haki ana mateso mengi,
lakini Bwana humwokoa nayo yote,
20 huhifadhi mifupa yake yote,
hata mmoja hautavunjika.
21 Ubaya utamuua mtu mwovu,
nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
22 Bwana huwakomboa watumishi wake,
yeyote anayemkimbilia yeye
hatahukumiwa kamwe.
*^ Zaburi hii imetungwa kila mstari ukianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22.