Zaburi 6
Sala Kwa Ajili Ya Msaada Wakati Wa Taabu
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Mtindo wa sheminithi.* Sheminithi ni mtajo mmojawapo katika lugha ya uimbaji. Zaburi ya Daudi.
Ee Bwana, usinikemee katika hasira yako,
wala usiniadhibu katika ghadhabu yako.
Unirehemu Bwana,
kwa maana nimedhoofika;
Ee Bwana, uniponye,
kwa maana mifupa yangu
ina maumivu makali.
Nafsi yangu ina uchungu mwingi.
Mpaka lini, Ee Bwana, mpaka lini?
 
Geuka Ee Bwana, unikomboe,
uniokoe kwa sababu ya fadhili zako.
Hakuna mtu anayekukumbuka
akiwa amekufa.
Ni nani awezaye kukusifu
akiwa kuzimu?
 
Nimechakaa kwa kulia kwa huzuni;
usiku kucha nafurikisha
kitanda changu kwa machozi;
nimelowesha viti vyangu vya fahari
kwa machozi.
Macho yangu yamedhoofika kwa kuhuzunika,
yamedhoofika kwa sababu ya adui zangu wote.
 
Kaeni mbali nami, ninyi nyote mtendao mabaya,
kwa maana Bwana amesikia kulia kwangu.
Bwana amesikia kilio changu kwa huruma,
Bwana amekubali sala yangu.
10 Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika,
watarudi nyuma kwa aibu ya ghafula.

*^ Sheminithi ni mtajo mmojawapo katika lugha ya uimbaji.