3
Moabu Wanaasi
Yehoramu* Yehoramu wakati mwingine limetajwa kama Yoramu. mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye akatawala kwa miaka kumi na miwili. Akafanya maovu machoni pa Bwana, lakini sio kama baba yake na mama yake walivyokuwa wamefanya. Akaondoa nguzo ya ibada ya Baali ambayo baba yake alikuwa ameitengeneza. Hata hivyo akashikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, wala hakuziacha.
Basi Mesha mfalme wa Moabu akafuga kondoo, naye akawa ampatie mfalme wa Israeli wana-kondoo 100,000 pamoja na sufu ya kondoo dume 100,000. Lakini baada ya Ahabu kufa, mfalme wa Moabu aliasi dhidi ya mfalme wa Israeli. Kwa hiyo wakati ule Mfalme Yehoramu akaondoka kutoka Samaria na kukusanya Israeli yote tayari kwenda vitani. Akapeleka pia ujumbe ufuatao kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda: “Mfalme wa Moabu ameasi dhidi yangu. Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Moabu?”
Akajibu, “Nitakwenda pamoja nawe. Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
Akauliza, “Je, tutashambulia kupitia njia gani?”
Akajibu, “Kupitia Jangwa la Edomu.”
Hivyo mfalme wa Israeli akaondoka akiwa pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kuzunguka kwa siku saba, jeshi likawa limeishiwa maji kwa matumizi yao na kwa ajili ya wanyama waliokuwa nao.
10 Mfalme wa Israeli akamaka, “Nini! Je, Bwana ametuita sisi wafalme watatu ili tu kututia mikononi mwa Moabu?”
11 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Bwana hapa, ili tuweze kumuuliza Bwana kupitia kwake?”
Afisa mmoja wa mfalme wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yuko hapa. Ndiye alikuwa akimimina maji juu ya mikono ya Eliya.”
12 Yehoshafati akasema, “Neno la Bwana liko pamoja naye.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli na Yehoshafati pamoja na mfalme wa Edomu wakamwendea.
13 Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina nini mimi nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.”
Mfalme wa Israeli akajibu, “La hasha, kwa sababu ni Bwana ambaye ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.”
14 Elisha akasema, “Hakika, kama Bwana Mwenye Nguvu Zote aishivyo ambaye ninamtumikia, kama si kuheshimu Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekutazama wala hata kukutupia jicho. 15 Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.”
Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa Bwana ukaja juu ya Elisha, 16 naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’ 17 Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Bwana: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ngʼombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa. 18 Hili ni jambo rahisi machoni pa Bwana. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu. 19 Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.”
20 Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji.
21 Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani. 22 Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu. 23 Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!”
24 Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga mpaka wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu. 25 Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri mpaka likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia vilevile.
26 Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu 700 wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa. 27 Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.

*3:1 Yehoramu wakati mwingine limetajwa kama Yoramu.