12
Maono Ya Paulo Na Mwiba Aliokuwa Nao
Yanipasa nijisifu, ingawa haifaidi kitu. Nitaenda kwenye maono na ufunuo kutoka kwa Bwana. Namjua mtu mmoja katika Kristo ambaye miaka kumi na minne iliyopita alichukuliwa juu hadi mbingu ya tatu. Kama ni katika mwili au nje ya mwili, sijui, Mungu ajua. Nami najua ya kwamba mtu huyu, kwamba ni katika mwili au nje ya mwili mimi sijui, lakini Mungu ajua, alinyakuliwa hadi Paradiso.* Paradiso hapa ina maana mbinguni. Huko alisikia mambo yasiyoelezeka, mambo ambayo binadamu hana ruhusa ya kuyasimulia. Nitajisifu kwa ajili ya mtu kama huyo, lakini sitajisifu kuhusu mimi mwenyewe ila mimi nitajisifia udhaifu wangu. Hata kama ningependa kujisifu, sitakuwa mjinga, kwa maana nitakuwa nasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu yeyote asije akaniona mimi kuwa bora zaidi kuliko ninavyoonekana katika yale ninayotenda na kusema.
Ili kunizuia nisijivune kwa sababu ya ufunuo huu mkuu, nilipewa mwiba katika mwili wangu, mjumbe wa Shetani, ili anitese. Kwa habari ya jambo hili nilimsihi Bwana mara tatu aniondolee mwiba huu. Lakini aliniambia, “Neema yangu inakutosha, kwa kuwa uweza wangu hukamilika katika udhaifu.” Kwa hiyo nitajisifu kwa furaha zaidi kuhusu udhaifu wangu, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. 10 Hii ndiyo sababu, kwa ajili ya Kristo, nafurahia udhaifu, katika kutukanwa, katika taabu, katika mateso na katika shida, kwa maana ninapokuwa dhaifu, ndipo nina nguvu.
Wasiwasi Wa Paulo Kwa Wakorintho
11 Nimekuwa mjinga, lakini ninyi mmenilazimisha niwe hivyo. Kwa kuwa ilinipasa kusifiwa na ninyi, kwa sababu mimi si dhalili kuliko wale “mitume walio bora,” ingawa mimi si kitu. 12 Mambo yanayomtambulisha mtume wa kweli, yaani, ishara, miujiza na maajabu, yalifanywa miongoni mwenu kwa saburi nyingi. 13 Je, ninyi ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila tu kwamba mimi sikuwa mzigo kwenu? Nisameheni kwa kosa hili!
14 Sasa niko tayari kuja kwenu kwa mara hii ya tatu, nami sitawalemea, kwa sababu sitahitaji chochote chenu, ila ninawahitaji ninyi, kwa kuwa hata hivyo watoto hawaweki akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi huweka akiba kwa ajili ya watoto wao. 15 Hivyo nitafurahi kutumia kila kitu nilicho nacho kwa ajili yenu, hata mwili wangu pia. Hata ingawa inaonekana ninavyozidi kuwapenda, ndivyo upendo wenu kwangu unavyopungua. 16 Iwe iwavyo, kwa vyovyote vile mimi sikuwalemea. Lakini kwa mimi kuwa mwerevu naliwapata. 17 Je, nilijipatia faida kwa kumtumia mtu yeyote niliyemtuma kwenu? 18 Nilimshawishi Tito aje kwenu, nami nilimtuma pamoja na ndugu yetu. Je, Tito aliwatumia ninyi ili kujipatia faida? Je, hatuenendi kwa roho moja, na hatuchukui hatua zile zile?
19 Je, mmekuwa mkifikiri kwamba sisi tunajaribu kujitetea mbele yenu? Sisi tumekuwa tukinena mbele za Mungu kama wale walio katika Kristo. Na chochote tufanyacho, ndugu wapendwa, ni kwa ajili ya kuwatia nguvu. 20 Kwa kuwa nina hofu ya kwamba nitakapokuja naweza kuwakuta nisivyotaka, nanyi mkanikuta msivyotaka. Nina hofu kwamba panaweza kuwa na ugomvi, wivu, ghadhabu, fitina, masingizio, masengenyo, majivuno na machafuko. 21 Nina hofu kwamba nitakapokuja tena kwenu, Mungu wangu atanidhili mbele yenu, nami nitasikitishwa na wengi waliotenda dhambi mbeleni, na wala hawajatubu kwa uchafu wao, uasherati, na ufisadi walioushiriki.

*12:4 Paradiso hapa ina maana mbinguni.