13
Mtu Wa Mungu Kutoka Yuda
Kwa neno la Bwana, mtu wa Mungu alifika Betheli kutoka Yuda wakati Yeroboamu alipokuwa amesimama kando ya madhabahu ili kutoa sadaka. Akapiga kelele dhidi ya madhabahu kwa neno la Bwana: “Ee madhabahu, madhabahu! Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Mwana aitwaye Yosia atazaliwa katika nyumba ya Daudi. Juu yako atawatoa dhabihu makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu wale ambao wanatoa sadaka hapa sasa, nayo mifupa ya wanadamu itachomwa juu yako.’ ” Siku iyo hiyo, mtu wa Mungu akatoa ishara: “Hii ndiyo ishara Bwana aliyotangaza: Madhabahu haya yatapasuka na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.”
Mfalme Yeroboamu aliposikia kile mtu wa Mungu alichosema, alipopiga kelele dhidi ya madhabahu huko Betheli, akanyoosha mkono wake kutoka madhabahuni na kusema, “Mkamate!” Lakini mkono aliokuwa ameunyoosha kumwelekea yule mtu ukasinyaa na kubaki hapo hapo, kiasi kwamba hakuweza kuurudisha. Pia, madhabahu yalipasuka na majivu yakamwagika sawasawa na ishara iliyotolewa na mtu wa Mungu kwa neno la Bwana.
Kisha mfalme akamwambia mtu wa Mungu, “Niombee kwa Bwana Mungu wako ili mkono wangu upate kupona.” Kwa hiyo mtu wa Mungu akamwombea kwa Bwana, nao mkono wa mfalme ukapona na kuwa kama ulivyokuwa hapo kwanza.
Mfalme akamwambia yule mtu wa Mungu, “Twende nyumbani kwangu upate chakula, nami nitakupa zawadi.”
Lakini yule mtu wa Mungu akamjibu mfalme, “Hata kama ungenipa nusu ya mali zako, nisingekwenda pamoja na wewe, wala nisingekula mkate au kunywa maji hapa. Kwa kuwa niliagizwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate wala usinywe maji au kurudi kwa njia uliyojia.’ ” 10 Kwa hiyo akafuata njia nyingine na hakurudi kupitia njia ile ambayo alikuwa ameijia Betheli.
11 Basi kulikuwepo na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme. 12 Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonyesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita. 13 Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda 14 na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?”
Akamjibu, “Mimi ndiye.”
15 Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi ule.”
16 Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa. 17 Nimeambiwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”
18 Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Bwana: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.) 19 Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.
20 Wakati walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu. 21 Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Umeasi neno la Bwana na hukushika amri uliyopewa na Bwana Mungu wako, 22 bali ulirudi na ukala mkate na kunywa maji mahali ambapo alikuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”
23 Wakati huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake. 24 Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, yule punda wake na simba wakiwa wamesimama karibu yake. 25 Baadhi ya watu waliopita pale waliona maiti imebwagwa pale chini, simba akiwa amesimama kando ya maiti, wakaenda na kutoa habari katika mji ambao nabii mzee aliishi.
26 Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu ambaye aliasi neno la Bwana. Bwana amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limemwonya.”
27 Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo. 28 Kisha akatoka akaenda akakuta maiti imebwagwa chini barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda. 29 Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika. 30 Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”
31 Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Wakati nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake. 32 Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Bwana dhidi ya madhabahu huko Betheli na dhidi ya madhabahu yote katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Samaria, hakika yatatokea kweli.”
33 Hata baada ya haya, Yeroboamu hakubadili njia zake mbaya, lakini mara nyingine tena akaweka makuhani kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu kutoka watu wa aina zote. Yeyote aliyetaka kuwa kuhani alimweka wakfu kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia miungu. 34 Hii ilikuwa ndiyo dhambi ya nyumba ya Yeroboamu ambayo iliisababishia kuanguka na kuangamia kwake hadi kutoweka kwenye uso wa dunia.